ANNUAL REPORT 2018

Taarifa ya Mwenyekiti

Kubadilisha maisha mtindo wa Safaricom

Kwa ufupi

Mwaka uliopita ulikuwa na changamoto tele kwa biashara nyingi kote nchini Kenya. Kwa mujibu wa ripoti za serikali, kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Kenya kilishuka hadi asilimia 4.9. Hii ilitokana na wasiwasi wa kisiasa uliokuwepo taifa hili lilipokuwa linakumbana na athari za kipindi kirefu cha uchaguzi.

Katika kipindi hicho, sekta ya utoaji wa mikopo ilishuhudia kiwango cha chini zaidi cha ukuaji kuwahi kushuhudiwa katika miaka 14. Hii ilichangiwa na sheria iliyoweka ukomo kwenye viwango vya riba pamoja na kupungua kwa shughuli za kiuchumi. Kadhalika, wateja walikabiliwa na ongezeko la bei ya vyakula kutokana na ukame wa muda mrefu ambao uliathiri uzalishaji katika sekta ya kilimo. Hili lilichangia kuongezeka kwa gharama ya maisha katika familia nyingi.

Hata hivyo, licha ya kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, ripoti za Serikali zinaonesha sekta ya Habari na Mawasiliano ilikua kwa asilimia 11 mwaka 2017. Ukuaji huu unatokana zaidi na kuimarika kwa uchumi wa kutumia mifumo wa kidijitali, biashara ya simu za rununu, na biashara ya kupitia mtandaoni, miongoni mwa mengine.

Upande wa washindani, tunaendelea kushuhudia mabadiliko mengi ambayo yanatarajiwa kuzua msisimko sokoni katika miezi michache ijayo. Tumeshuhudia kuingia sokoni kwa kampuni mpya za mawasiliano ya simu na zisizo za kutoa huduma ya mawasiliano ya simu moja kwa moja. Matukio haya ni ushahidi tosha wa jinsi soko letu linavyobadilika kila uchao, na anayefaidi zaidi bila shaka ni mteja.

Mazingira ya kisheria

Tukiangazia usimamizi wa sekta hii, tumekuwa tukifuatilia kwa karibu sana matukio katika mazingira ya kisheria na usimamizi. Tutaendelea kufanya hivyo kwa makini tukiendelea kutathmini msimamo wetu kuhusu mapendekezo yaliyo kwenye rasimu ya utafiti kuhusu sekta hii ambao ulikuwa umefanywa kwa niaba ya Mamlaka ya Mawasiliano Kenya.

Rasimu ya matokeo ya utafiti huo inapendekeza hatua kadha zichukuliwe ambazo hazijatufurahisha kamwe. Hatua hizi ni pamoja na majaribio ya kubadilisha hali ya mchezo uwanjani kwa kuanza kudhibiti bei pamoja na wahudumu kutakiwa kutumia miundo mbinu kwa pamoja.

Ingawa mapendekezo haya bado hayajaidhinishwa wala kuanza kutekelezwa, hali kwamba yametolewa ni ishara kwamba huenda tukawa tunaelekea katika kipindi ambacho mhudumu atakuwa anaadhibiwa kwa sababu ya ufanisi – ambao umepatikana kwa njia ya haki na kwa kutoa jasho, kupitia mkakati mwafaka wa kibiashara, uvumbuzi na uwekezaji wa busara.

Msimamo wetu ni kwamba soko linafaa kuwa huru na sekta ijidhibiti kwa nguvu zake za kawaida. Kadhalika wahudumu waachwe washauriane wenyewe kuhusu kutumia kwa pamoja miundo mbinu na mitambo kupitia makubaliano ya kibiashara, kama inavyofanyika kwa sasa.

Kuanza kudhibitiwa kwa bei sio tu kwamba kunaleta hatari ya wahudumu kuacha kuwekeza katika mifumo yao, wakisubiri kutumia mitambo ya wengine, bali pia ni hatua itakayomwathiri mteja mwishowe pamoja na kuathiri hadhi ya taifa hili kama kiongozi katika uvumbuzi.

Isitoshe, mapendekezo kwamba Safaricom itaruhusiwa tu kuanza kutoa huduma mpya iwapo huduma hiyo inaweza pia kutolewa na washindani wake na kwamba kampuni hii iwekewe masharti ikitaka kuzindua shughuli za mauzo na matangazo zinazowalenga wateja wa kiwango fulani, haya ni mambo yatakayoathiri uwezo wetu wa kuvumbua mambo mapya ya kumfaa mteja na pia kuathiri uwezo wetu wa kuwafikia wateja wengi. yakibiashara na kufanya kampeni za mauzo tukilenga wateja katika ngazi mbalimbali. Mapendekezo haya pia yanatushangaza ni vipi yanaweza kuwafaa zaidi ya watu 40 milioni na zaidi wanaotumia simu nchini. Hili ndilo jambo la msingi ambalo msimamizi yeyote wa sekta hii anafaa kuzingatia.

Kwa kuzingatia mambo haya yanayojiri, tutaendelea kushauriana na Mamlaka ya Mawasiliano tukitafuta suluhu ambayo itazifaa pande zote. Sekta ya mawasiliano ya simu nchini Kenya ni huru na ya ushindani, na wahudumu wanafaa kuachwa washindane wenyewe kwa kiwango cha ubora, bei na uvumbuzi kwenye bidhaa na huduma zao. Juhudi za kuanza kudhibiti bei ya rejareja ni za kurejesha watu nyuma, zisizowafaa wateja na zisizo za haki. Isitoshe, zinaenda kinyume na sera ya kiuchumi ya Kenya.

Mustakabali wa Kibiashara

Huku tukiendelea kuwashirikisha wadau wote, tutaendelea kuwekeza katika biashara yetu, tukiongozwa na lengo kuu la utambulisho wa nembo yetu ambalo ni Kubadilisha Maisha.

Lengo hili kuu linaongoza mkakati wetu ulio na nguzo tatu kuu ambazo ni kuweka maslahi ya wateja mbele, kutoa bidhaa na huduma zifaazo, na kuboresha uendeshaji wa shughuli zetu. Mkakati huu umeendelea kuzaa matunda mema. Tukitazama siku zijazo, tutaendelea kuwa imara katika kutekeleza mkakati huu na kukuza mali ya wenyehisa huku tukiendelea kujitolea kudumisha Mtindo wa Safaricom wa kuwa kampuni inayoongozwa na malengo, yenye kuangazia zaidi huduma kwa wateja na kuangazia matokeo mema. Huu ni mkakati wa muda mrefu ambao tayari unatuzalia matunda mema, na tunaamini kwamba una umuhimu mkubwa katika ukuaji wa biashara yetu.

Usimamizi wa kampuni

Katika mwaka uliomalizika, kulitokea mabadiliko kwenye bodi ya wakurugenzi. Mohamed Joosub, Till Streichert na Linda Muriuki waliteuliwa kujiunga na bodi.

Nawakaribisha wakurugenzi hawa wapya na kumshuruku sana John Otty, aliyejiuzulu Mei 8, 2018, kwa mchango wake kipindi alichokuwa mwanachama wa bodi. Nina furaha pia kumkaribisha tena kazini Afisa Mkuu Mtendaji wetu, Bob Collymore, kutoka likizo yake ya kimatibabu.

Aliendelea kutoa uongozi muhimu kwa kampuni hii na kufanya kazi kwa karibu sana na Bodi yetu ya Wakurugenzi na Kamati Tendaji. Hili lilichangia pakubwa matokeo mazuri ambayo tuliyapata mwaka uliomalizika. Kwa niaba ya Bodi, ningependa kuwashukuru wanahabari, washirika wetu na umma kwa jumla kwa kuheshimu haki ya faragha ya Bob na maisha yake alipokuwa likizoni.

Nikihitimisha, ningependa pia kuwashukuru wafanyakazi na wasimamizi wa Safaricom kwa kujitolea kwao kuendelea kutimiza lengo letu la kubadilisha maisha ya watu.

Tunatarajia mwaka mwingine mzuri wa kubadilisha maisha ya watu na kushirikiana kuhakikisha ufanisi, kwani tunapoungana pamoja, mambo makuu yanawezekana.

Nicholas Ng'ang'a

Mwenyekiti