ANNUAL REPORT 2018

Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu

Lengo, watu na faida

Safaricom ipo kwa ajili ya kubadilisha maisha ya watu. Hili ndilo lengo letu kuu; jambo linalotupa msukumo katika kila tunalolitenda. Ndilo jambo linalotuongoza na kutuelekeza katika kutekeleza mkakati wetu ambao una msingi wake katika nguzo tatu kuu, kupatia kipaumbele maslahi ya wateja wetu, kutoa bidhaa na huduma zinazofaa, na kuendesha shughuli zetu kwa njia bora zaidi. Katika mwaka uliopita, tulidhihirisha kujitolea kwetu katika kutekeleza mkakati huu, ambapo tuliweza kuhimili changamoto za kiuchumi na kisheria na kuandikisha matokeo mazuri ya kifedha. Kadhalika, tuliongeza thamani kwa uwekezaji wa wenyehisa wetu na kubadilisha maisha ya mamilioni ya Wakenya kila siku.

Katika mwaka huo pia, nilichukua likizo kwenda kupokea matibabu maalum. Hata hivyo, niliendelea kufanya kazi kwa karibu sana na kundi la maafisa wangu watendaji kupitia mikutano ya ana kwa ana London na mingine ya mbali kwa kutumia teknolojia ya mtandao. Tulifanikiwa kuiongoza na kuielekeza kampuni hii kupitia kipindi chenye changamoto tele. Walipokuwa wanasimamia shughuli za kila siku za biashara yetu, nilipata muda wa kutafakari kuhusu jambo ambalo nimekuwa ninalithamini sana: utamaduni wa kampuni yetu.

Safaricom ni kampuni inayoandikisha matokeo mema sana, ikisaidiwa na wanaume na wanawake 6,000 waliojitolea kuhakikisha kwamba tunatimiza lengo la nembo yetu la kubadilisha maisha ya watu. Lakini mara nyingi huwa tunasahau kuangazia moja ya viungo muhimu ambavyo huchangia ufanisi wetu, na kiungo hiki ni watu. Wanaume na wanawake hawa, ambao wengi wa wenyehisa wetu na wadau wengine huwa hawakutani nao hata kidogo, ndio kiungo ambacho ni siri ya mafanikio yetu, ndiyo injini inayosukuma ukuaji wetu.

Watu na utamaduni

Ni kupitia kuwekeza katika kundi la wafanyakazi imara na wenye ujuzi ufaao ambapo kampuni yetu imeendelea kuongoza katika sekta hii, wakiongozwa na mkakati wetu. Kwa hivyo mwaka huu, tutaanza kuangazia
kuboresha utamaduni wa kampuni yetu kusaidia kutimiza malengo yetu ya kibiashara, kwa kuangazia mambo manne makuu: lengo, utu, ukuaji na kuaminika. Tupo kwenye safari ya kuunda pahala pa kufanyia kazi ambapo panaendeleza utendakazi bora, kwa kuanza kukidhi mahitaji ya wafanyakazi wetu.

Tumeanza kufanya hivyo kwa kuwekeza zaidi katika maslahi ya wafanyakazi kupitia kampeni yetu ya Utu Kazini 100%, ambayo lengo lake ni kuhamasisha kampuni mbalimbali kuwatambua wafanyakazi wao kama watu, na sio rasilimali, ili kuwa na kikosi cha wafanyakazi wenye furaha, wenye afya na wenye utendaji kazi bora.

Baada ya kupata wakati wa kutafakari kuhusu mchango wa afya bora na hali nzuri, na ustawi wa wafanyakazi kwa kampuni, nina hamu sana ya kuwekeza katika miradi ambayo itahakikisha tunaendelea kuongeza thamani kwa uwekezaji wa wenyehisa wetu na kuendelea kubadilisha maisha ya watu.

Kuwajumuisha wote

Kama kampuni, tumejitolea pia kuendelea kukubali tofauti zilizopo katika jamii na kuwajumuisha watu wote. Hii ina maana tutawapandisha vyeo wanawake zaidi wachukue nyadhifa za uongozi, na pia tutawaajiri watu wengi walio na ulemavu katika kampuni yetu.

Tunajionea fahari kwamba tumetimiza kiwango cha 1:1 wanaume kwa wanawake miongoni mwa wafanyakazi wetu. Sasa, ipo haja ya kuunda nafasi zaidi kwa wanawake kuwawezesha kuingia katika nafasi za uongozi. Kuambatana na hili, tumejitolea kuhakikisha tuna idadi sawa ya wanawake na wanaume katika nyadhifa za juu za usimamizi wa kampuni kufikia 2020.

Kadhalika, tumeahidi kuongeza idadi ya wafanyakazi wetu walio na ulemavu kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 1.7 hadi asilimia tano kufikia Machi 2021, na kufanya kazi kwa karibu sana na washirika wetu kutetea kujumuishwa kikamilifu kwa watu wenye ulemavu serikalini na katika sekta ya kibinafsi.

Kutekeleza Mkakati

Katika Safaricom, huwa twapenda kuzungumzia nguzo tatu kuu (3P) zinazoongoza mkakati wetu: Lengo, Watu na Faida – kwamba unapoweka lengo lako kuu na maslahi ya watu mbele, faida hufuata.

Ni mtazamo huu ambao umetuwezesha kuandikisha matokeo mazuri ya kifedha kila mwaka, tukijikumbusha kwamba kampuni yetu ipo kwa ajili ya kubadilisha maisha ya watu; kuanzia kwa jamii ambazo twatumikia na kuhudumia hadi kwa wafanyakazi wetu.

Chini ya uongozi wa kundi letu thabiti la viongozi na wafanyakazi waliojitolea, tulipanua huduma tunazotoa ili kusaidia mapato ambayo hutokana na kupigwa kwa simu na kutumwa kwa SMS, huduma ambazo ziliendelea kujitenga na mtindo kwingineko duniani na kuandikisha ukuaji wa pamoja wa kuridhisha wa 2.9% mwaka baada ya mwaka. Licha ya matokeo haya mazuri, tunatambua kwamba matumizi ya huduma za kupiga simu na kutuma SMS yanapungua duniani, na tunajiandaa kwa hilo kama kampuni kwa kuvumbua huduma na bidhaa mpya.

Tunatarajia siku zijazo mteja awe na usemi zaidi katika huduma za data na kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu, yote haya yakichangiwa na thamani ambayo tutakuwa tunaendelea kuitoa kwa wateja. Kwa kutambua mtindo huu, tunabadilisha muundo wa biashara yetu na kuifanya kuweza kuhimili mabadiliko na kuiwezesha kuhakikisha inapata ukuaji endelevu kwa kutumia fursa mpya katika huduma ya data kupitia simu na nyaya, na huduma ya kutuma, kupokea pesa na kufanya malipo kwa njia ya simu.

Huku hitaji la huduma hizi likiendelea kuongezeka, tunajiweka katika nafasi nzuri ya kutumia fursa zitakazochipuka ili kuweza kupunguza pengo la kutofikiwa kwa huduma zetu ambalo limekuwepo kutokana na changamoto za umbali wa maeneo miongoni mwa sababu nyingine.

Tunafanya hivyo kupitia: kuendelea kuwekeza katika kupanua upatikanaji wa huduma yetu ya 4G, kutoa huduma ya mtandao ya kasi na ya kutegemewa kwa wateja wa rejareja na wa kibiashara kupitia huduma za mtandao wa kupitia Safaricom Business na Safaricom Home; na kujenga ushirikiano na wadau wengine ambao utatuwezesha kutoa habari na makala za ubora wa hali ya juu za ndani ya nchi na za kimataifa.

Katika mwaka wa kifedha uliomalizika, tuliendeleza juhudi zetu za kuifanya huru M-PESA kwa kupunguza ada inayotozwa wafanyabiashara wanaotumia Lipa Na M-PESA kwa asilimia 50, na pia kwa kufuta kabisa ada iliyokuwa inatozwa kiasi cha pesa cha chini ya KES 200 ili kuwahamasisha watu zaidi kutumia huduma hii. Tunaitazama hii kama fursa kubwa ambayo bado haijatumiwa vyema. Tunaendelea pia kuimarisha na kurahisisha mambo kwa wateja wakitumia M-PESA kupitia kuboresha mfumo wenyewe, kuimarisha viungo vya usalama na kupitia mySafaricom App, ili kuhakikisha uendelevu wa muda mrefu wa mfumo na huduma hiyo muhimu kwa biashara yetu.

Kama sehemu ya juhudi zetu zinazoendelea za kutoa huduma na bidhaa mpya za kubadilisha mambo sokoni, tunajizatiti pia kuhakikisha ufanisi wa Masoko, huduma ya kufanya biashara kidijitali ambayo tuliizindua mwaka jana. Tunakusudia kufanya hivi kwa kulainisha shughuli zake kukidhi mahitaji sokoni na kuhakikisha inabadilisha mambo katika biashara ya mtandaoni Kenya. Nje ya nchi, tunaendelea kufuatilia na kuchunguza fursa mpya kuambatana na mkakati wetu, ambao tuliufungamanisha na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) mwaka 2016.

Maendeleo Endelevu

Kwa kutambua ukweli kwamba biashara yetu haiwezi kufanikiwa bila kujali jamii katika maeneo ambayo huwa tunatoa huduma zetu, tumekumbatia na kuanza kufanikisha kutimizwa kwa tisa kati ya Malengo yote 17 ya Maendeleo Endelevu (SDG): Afya Njema & Ustawi wa Watu (Lengo 3); Elimu Bora (Lengo 4); Nishati Mbadala kwa Gharama Nafuu (Lengo 7); Ajira yenye staha & Ukuaji wa Uchumi (Lengo 8); Viwanda, Uvumbuzi & Miundo mbinu (Lengo 9); Kupunguza Ukosefu wa Usawa (Lengo 10); Matumizi na & Uzalishaji wenye Uwajibikaji (Lengo 12); Amani, Haki & Taasisi Madhubuti (Lengo 16) na Ushirikiano ili Kutimiza Malengo (Lengo 17).

Malengo haya yanaashiria kujitolea kwetu kuchangia juhudi za ulimwengu katika kutimiza malengo haya ya ustawi kwa wote, na ni fursa kwa kampuni yetu kutekeleza mchango zaidi katika kuhakikisha ukuaji wa kiuchumi na kijamii kwa njia ya usawa. Tukiongozwa na SDG hizi, tunawekeza katika miradi inayobadili maisha ya watu, kushirikiana na washirika wetu kutoa huduma muhimu katika sekta kama vile afya, elimu na kilimo na kuwawezesha vijana Kenya.

Katika siku zijazo, tunatarajia fursa nyingi za ukuaji endelevu. Moja ya malengo yetu ni kuibadilisha Safaricom na kuwa kampuni inayoweza kuchukua hatua upesi, kwa kuunda mazingira yanayowezesha maamuzi kufanywa kwa haraka na makosa kutazamwa kama fursa za kujifunza haraka. Yote haya huanza kwa kuwekeza katika wafanyakazi wetu, ambao wana jukumu la kuhakikisha kwamba Safaricom inasalia kuwa kampuni ya mawasiliano ya simu inayoongoza, na wanaotudhihirishia kila siku kwamba tunapoungana pamoja, mambo makuu huwezekana.

Twaweza!

Bob Collymore

Mkurugenzi Mkuu