Lengo – Kubadilisha Maisha

Katika mwaka tunaouangazia, tulikuwa imara katika kuongozwa na lengo letu la Kubadilisha Maisha. Tulidhihirisha hilo kupitia njia nne kuu, ambazo ni:

  • Uandaaji wa bidhaa na huduma kama vile Boost ya Biashara
  • Kusaidia jamii moja kwa moja kupitia vifaa na teknolojia zifaazo, na kuwasaidia wanajamii kutimiza uwezo wao kupitia Wakfu wa M-PESA na Wakfu wa Safaricom
  • Kusaidia kutimiza mahitaji ya jamii kupitia Ndoto Zetu, kwa kusaidia Wakenya waliostahili kutimiza ndoto zao
  • Kujitolea kwetu kuhakikisha uwazi na uwajibikaji kwa kuchapisha maelezo kuhusu shughuli zetu za kibiashara na nyinginezo katika Ripoti ya Uendelevu ya kumi na mbili

Tumeonyesha moja kwa moja nguvu ya mabadiliko inayopatikana kwa kutumia vyema teknolojia kubadilisha maisha, kujenga thamani ya pamoja, kuongoza mabadiliko ya manufaa, na kutoa suluhu kwa changamoto zinazoikabili jamii

Matokeo ya Biashara

Inaridhisha sana kwamba ukuaji ambao tumeushuhudia katika kipindi tunachokiangazia umekuwa mpana, kwani hii ina maana kwamba injini za ukuaji zinafanya kazi sawa sawa. Hili, ukilizingatia pamoja na kasi ya ukuaji ambao tunaupata Ethiopia, linaendana vyema na thamani kubwa ambayo tunatarajia Kampuni itaweza kuhakikisha inapatikana katika kipindi cha wastani hadi kipindi kirefu.

Kwa maelezo zaidi kuhusu matokeo yetu ya kifedha na shughuli zetu Ethiopia, Bonyeza hapa na Bonyeza hapa mtawalia.

Mwaka tunaouangazia ulikuwa kipindi cha wakati mgumu sana kwa shughuli zetu Kenya na Ethiopia. Viwango vya juu vya riba na mfumko wa bei vilizalisha mazingira magumu sana mwaka huo, hata licha ya ukuaji mzuri wa GDP wa 5.6% mwaka 2023 nchini Kenya.

Kudorora kwa thamani ya sarafu pamoja na kukazwa kwa sera ya kifedha nchini Kenya, na kudhibitiwa kwa sarafu nchini Ethiopia vilizidisha makali ya changamoto hizo, na kuathiri bei ya kawi. Hili nalo lilizidisha shinikizo za mfumko wa bei na kupunguza kiasi cha fedha za matumizi ya hiari miongoni mwa watu.

Ni muhimu kueleza kuwa haya yote yalikuwa yakitokea katika mazingira ya uchumi wa dunia ambao ulikuwa bado wenye misukosuko, ambapo vita na athari zake kwenye biashara, uchukuzi na kawi viliendelea kuongeza shinikizo kote duniani na hasa katika mataifa yanayoendelea kiuchumi.

Kwa maelezo zadi kuhusu mazingira yetu ya uendeshaji shughuli, Bonyeza hapa.

Changamoto nyingine ilitoka upande wa kisheria, ambapo tulishuhudia kuongezwa kwa viwango vya kodi ya bidhaa katika miamala ya kutuma pesa kwa njia ya simu na pia kodi ya ziada kwenye laini za simu. Tunaendelea kufuatilia kwa karibu yanayotokea, ukizingatia kwamba kuongezwa kwa kodi kunaweza kuathiri biashara yetu na shughuli zetu.

Baada ya Bodi kuidhinisha mkakati wetu wa 2030, lengo letu sasa ni kuwa kampuni ya kiteknolojia inayoongozwa na malengo inayoongoza Afrika. Kwa kuongozwa na ruwaza hii, tunalenga kutumia kikamilifu fursa ambazo tumezitambua.

Miongozi mwa fursa hizi ni kasi ya kibiashara ambayo tunaitarajia nchini Ethiopia kuanzia kipindi kifupi hadi cha wastani. Hii ni pamoja na ongezeko la idadi ya watu wanaotumia mtandao wetu, fursa za kufaidi kifedha kama vile data kwenye simu – ambayo tumeshuhudia ongezeko kubwa katika utumiaji wake – kuongezeka kwa wanaotumia M-PESA, na kusambazwa zaidi kwa huduma zetu kote nchini humo kutokana na kuwepo mazingira yenye usalama. Tunatambua na kuthamini sana usaidizi na ushirikiano wa serikali ya Ethiopia tunapofanya kazi kwa pamoja kuisaidia kutimiza azma yake ya kujenga Ethiopia ya Dijitali.

Ethiopia ni ya pili kwa idadi ya watu barani, na wengi ni vijana. Hata hivyo, matumizi ya simu ni 50% pekee, jambo linaloashiria uwezo mkubwa wa soko hilo. Tuliufunga mwaka huo tukiwa na vituo 2,800 vya mitambo ya kutoa huduma za mawasiliano na tunatarajia kwamba tutakuwa tumeongeza maeneo 3,500 kwenye mtandao wetu kufikia mwisho wa mwaka wa kifedha wa 2025. Hili litawezesha kutimizwa kwa lengo letu la kuwa mstari wa mbele katika ukumbatiaji wa dijitali na ujumuishaji wa wengi katika mifumo ya kifedha katika soko hilo.

Ukizingatia kwamba biashara yetu ya huduma za mtandao Kenya tayari imekomaa, tunaiona fursa katika huduma za kifedha kwa njia ya simu, jambo litakalotuwezesha kufikishia wengi huduma za kifedha na kuhakikisha watu wengi wanajumuishwa katika mifumo ya kifedha. Tunaiendeleza M-PESA ili kuifanya kuwa jukwaa linalotoa huduma za usimamizi wa mali, na huduma mbalimbali za mikopo na uwekaji akiba.

Tunafanya kazi pamoja na serikali kusaidia kufanywa dijitali kwa huduma za serikali na kurahisisha utoaji huduma kwa raia. Kwa pamoja na wadau wengine katika sekta hii na kwa usaidizi wa Serikali ya Kenya, tulizindua kiwanda cha kipekee cha kufunganisha mitambo Kenya ambacho kitazalisha simu za kisasa na mitambo mingine, na kuifanya kuwa rahisi kutimiza ajenda ya Serikali ya uchumi wa dijitali.

Kwa maelezo zaidi kuhusu mkakati wetu, Bonyeza hapa.

Katika mwaka huo, tulishuhudia ukuaji mkubwa katika biashara yetu ya huduma za mtandao, pamoja na data kwa njia ya simu. Katika data kwa njia ya simu, simu za bei nafuu ambazo tunazitengeneza kupitia kiwanda chetu zimeanza kuonyesha matokeo – ishara nyingine kwamba tunatoa huduma sahihi na zifaazo kwa wateja wetu.

Kwa kuligawa soko kwa busara, na kuangazia sehemu mbalimbali za soko kwa huduma wanazohitaji zaidi, tumekuwa tukiongeza matumizi ya akili bandia, au AI, na pia data katika kuongoza maamuzi. Tunachochea ukuaji na uvumbuzi kwa biashara kubwa na pia biashara ndogo na za wastani (MSMEs) kupitia huduma bora na za gharama nafuu za Teknolojia ya Mtandao katika Kila Kifaa (IoT) na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT). Miongoni mwa suluhu nyingine kwa biashara, tunaimarisha suluhu za tarakilishi kwenye wingu, yaani cloud, na usalama wa mtandaoni, kwa kuzifungamanisha na bidhaa zetu za huduma za mtandao. Kadhalika, tunasaidia MSMEs na suluhu kama vile mipango ya kutekeleza dijitali katika SME ambayo hutoa vifaa vya uzalishaji vilivyowezeshwa kutumia teknolojia ya tarakilishi kwenye wingu, yaani cloud.

Kwa maelezo zaidi kuhusu teknolojia na huduma zetu, Bonyeza hapa na Bonyeza hapa mtawalia.

Tunaamini kwamba tumefanikiwa kuongeza matumizi kwa kuangazia:

  • Mahitaji hasa ya wateja
  • Jinsi wanavyoingiliana na huduma zetu
  • Safari wanazozichukua wakiwa nasi

Tunaamini ukuaji huu umetokana na filosofia yetu ya kuangazia mteja katika kila jambo, pamoja na mpango unaoendelea wa kupunguza bei za bidhaa zetu katika vitengo vyote kwa kati ya 40% na 60% katika miaka minne iliyopita.

Teknolojia imekuwa kiungo muhimu katika maisha yetu ya kila siku, ambapo inaongoza uvumbuzi na maendeleo katika sekta mbalimbali za uchumi, na kubadilika kwetu kutoka kampuni ya mawasiliano hadi kampuni ya kiteknolojia kunaongozwa na kujitolea kwetu kuziba mapengo yaliyopo katika kufikia huduma za kidijitali na za kifedha. Kwa kudhihirisha uwezo wetu wa kutumia teknolojia kutoa suluhu zinazotatua shida mbalimbali kwenye jamii, tumetilia mkazo safari yetu ya kimkakati ya kuwa kampuni ya teknolojia.

Kwa maelezo zaidi kuhusu kuangazia mteja, Bonyeza hapa.

Inafurahisha kueleza kwamba mfumo ikolojia wa Kampuni yetu umepangwa sawa kuhakikisha ukuaji. Tumeweka mikakati ya kufanikisha hili kupitia matumizi bora ya rasilimali na upunguzaji wa gharama kupitia teknolojia, miundo mbinu, na pia kujitolea kutimiza maadili ya uhifadhi wa mazingira. Kwa sasa, nishati ya jua au sola, tayari inatumika kuendesha 24% ya mitambo yetu ya mawimbi ya mawasiliano.

Kwa maelezo zaidi kuhusu matokeo yetu ya kifedha, Bonyeza hapa.

Tumekuwa tukihudumu Ethiopia kwa takriban miezi 18, na najivunia sana hatua ambazo tumezipiga nchini humo. Lengo letu limekuwa kupanua shughuli zetu ili kujiweka katika nafasi muhimu kwenye sekta ya mawasiliano ya simu nchini humo kama tunavyotazamia.

Kwa sasa, tumefikia 40% ya wananchi nchini humo na tumeongeza wateja wetu hadi zaidi ya 9.4 milioni tangu kuanza shughuli zetu. Lengo letu la kutekeleza mchango muhimu katika kuifanya Ethiopia kuwa ya kidijitali bado lipo, kupitia miundo mbinu na matumizi, mambo yanayodhihirisha kwamba tupo katika nafasi nzuri ya ukuaji nchini humo.

Ni fahari yangu kukariri kuwa kujitolea kwa Safaricom kwa watu katika maeneo tunayohudumu, na kwa mazingira kote tunakoishi, kulisalia imara katika mwaka tunaouangazia. Katika kipindi cha mwaka mmoja, taifa lilitoka kwa kiangazi na kuingia kwenye mafuriko, jambo ambalo lenyewe ni ushahidi wa athari za mabadiliko ya tabia nchi. Ni heshima yangu kuweza kuongoza uwakilishi wa sekta ya kibinafsi katika Mfuko wa Msaada wa Kukabiliana na Janga la Taifa, na kusaidia juhudi za serikali.

Nyakfu zetu mbili ziliendeleza kazi yake muhimu katika kutatua changamoto za kiafya, kielimu na kifedha na ujumuishaji. Usaidizi na uvumbuzi ambao nyakfu hizo hutoa vinasalia kuwa sehemu muhimu ya jukumu letu kama shirika raia wa kuwajibika.

Isitoshe, udhamini wetu wa shindano la kandanda la Chapa Dimba mwaka huu uliwawezesha maelfu ya vijana kutoka timu 3,300 kote nchini, kutimiza ndoto yao kuhusu mchezo huo. Inaridhisha sana kuwaona wakikutana na kujumuika kupitia michezo na muziki na kuendeleza vipaji vyao.

Kwa maelezo zaidi kuhusu nyakfu zetu, CSI na mazingira, Bonyeza hapa na Bonyeza hapa mtawalia.

Ninaamini kwamba tupo kwenye nafasi nzuri ya kuendelea kwenye mkondo wetu wa ukuaji thabiti katika kipindi kifupi, cha wastani na kirefu. Katika kipindi cha wastani, ninatarajia kwamba tutaanza kutengeneza faida nchini Ethiopia kufikia mwisho wa mwaka wa nne wetu kuwa na shughuli zetu humo.

Nchini Kenya, kwa azma yetu ya kubadilisha maisha, sasa tunatekeleza ruwaza na mkakati mpya. Tutaendelea kushuhudia ukuaji, tunapojizatiti kuwa kampuni ya kiteknolojia inayoongoza Afrika kufikia 2030.

Ninaamini kwamba kwa njia zetu za wepesi wa kufanya kazi na kuchukua hatua, utamaduni wetu wa kuangazia mteja katika kila kitu na kuwa na manufaa kwa jamii, tunao msukumo, nguvu na vifaa vya kuimarisha zaidi ukuaji ambao tumeupata mwaka huo.

Ninaishukuru sana Bodi yetu mpya kwa jinsi walivyoniunga mkono kwa kujitolea, bidii na umakinifu na bila shaka kundi lote la wasimamizi. Uongozi wao wa hekima umetupatia msingi imara ambao umetuwezesha kufanikisha matokeo ya kuridhisha ambayo tumeyaona.

Ningependa pia kushukuru mamlaka simamizi za sekta yetu nchini Kenya na Ethiopia, ambazo uungaji mkono wake ni muhimu sana katika jinsi tunavyoendesha shughuli zetu. Wauzaji wa bidhaa na huduma zetu na maajenti katika mataifa hayo mawili, pia, wameendelea kuchangia pakubwa katika ufanisi wetu. Ningependa kuwashukuru kwa uaminifu wao na kwa kujitolea kukuza nembo yetu.

Kwa wenzangu kote katika biashara yetu – ninajivunia sana kujitolea kwenu, vipaji na kwa kufuata mtindo wetu wa ufanyaji kazi, kuangazia mteja katika kila jambo na kujitolea kwetu kubadilisha maisha. Ni juhudi zetu ambazo zimetuwezesha kufanikisha matokeo haya.

Ningependa kuwashukuru wenyehisa wetu wote, na washirika wetu wote pamoja na wadau ambao wameendelea kutuunga mkono, jambo ambalo ni muhimu sana kwa biashara yetu.

Mwisho kabisa, ningependa kuwashukuru wateja wetu kwa uaminifu wao katika mwaka ambao ninajua umekuwa mgumu sana kwa wateja wetu. Tunathamini sana imani yenu kwetu kuwapa huduma na bidhaa mnazozihitaji.

Peter Ndegwa
Afisa Mkuu Mtendaji